John 6:1-14

Yesu Alisha Wanaume 5,000

(Mathayo 14:13-21; Marko 6:30-44; Luka 9:10-17)

1 aBaada ya haya, Yesu alikwenda ngʼambo ya Bahari ya Galilaya, ambayo pia huitwa Bahari ya Tiberia. 2 bUmati mkubwa wa watu uliendelea kumfuata, kwa sababu waliona ishara nyingi za miujiza alizofanya kwa wagonjwa. 3 cKisha Yesu akapanda mlimani akaketi huko pamoja na wanafunzi wake. 4 dPasaka ya Wayahudi ilikuwa imekaribia.

5 eYesu alipotazama na kuuona ule umati mkubwa wa watu ukimjia, akamwambia Filipo, “Tutanunua wapi mikate ili watu hawa wale?” 6Aliuliza swali hili kumpima, kwa maana alishajua la kufanya.

7 fFilipo akamjibu, “Hata fedha kiasi cha dinari mia mbili,
Dinari 200 ni sawa na mshahara wa kibarua wa siku 200; mshahara wa kibarua ulikuwa dinari moja kwa siku.
hazitoshi kununua mikate ya kuwapa watu hawa ili kila mtu apate kidogo.”

8 hMmoja wa wanafunzi wake aitwaye Andrea, ndugu yake Simoni Petro, akamwambia, 9 i“Hapa kuna mvulana mmoja mwenye mikate mitano ya shayiri na samaki wawili wadogo. Lakini hivi vitatosha nini kwa umati huu wote?”

10Yesu akasema, “Waketisheni watu chini.” Palikuwa na majani mengi katika eneo lile, nao watu wakaketi. Palikuwa na wanaume wapatao 5,000. 11 jNdipo Yesu akachukua ile mikate, akamshukuru Mungu na kuwagawia wale watu waliokuwa wameketi. Akafanya vivyo hivyo na wale samaki. Kila mtu akapata kadiri alivyotaka.

12Watu wote walipokwisha kula na kushiba, akawaambia wanafunzi wake, “Kusanyeni vipande vilivyobaki vya ile mikate, kisipotee chochote.” 13Hivyo wakavikusanya, wakajaza vikapu kumi na viwili kwa vipande vya ile mikate mitano ya shayiri na samaki wale wawili wadogo vilivyobakishwa na waliokula.

14 kBaada ya watu kuona muujiza ule Yesu aliofanya, walianza kusema, “Hakika huyu ndiye Nabii ajaye ulimwenguni!”
Copyright information for SwhNEN